KUTAMBUA FURSA ZINAZOLETWA NA MUNGU


 Kitabu cha Matendo kimejaa visa vinavyoeleza jinsi wanafunzi walivyotumia fursa zilizoletwa na Mungu kupanua ufalme Wake. Tangu mwanzo hadi mwisho wa kitabu, tunasoma visa vinavyosisimua vya kanisa la awali na jinsi lilivyokua, licha ya kukabiliwa na changamoto za ndani na nje. 


 Katika 2 Wakorintho 2: 12, 13, kwa mfano, mtume Paulo anasimulia uzoefu wake akiwa Troa: " Basi, nilipofika Troa kwa ajili ya Injili ya Kristo, nikafunguliwa mlango katika Bwana, sikuona raha nafsini mwangu, kwa sababu sikumwona Tito ndugu yangu, bali niliagana nao, nikaondoka kwenda Makedonia ." Kwa njia ya muujiza, Mungu alimfungulia Paulo mlango wa kuhubiri injili katika bara la Ulaya, na alijua kuwa milango ambayo Mungu anaifungua leo yaweza kufungwa kesho . Kwa kutumia fursa na kwa kuona uwezekano, alisafiri mara moja kwa meli kuelekea Makedonia . 


 Mungu wa Agano Jipya ni Mungu wa mlango ulio wazi Mungu ambaye kwa uongozi Wake anatupatia fursa za kutangaza imani yetu. Katika kitabu chote cha Matendo, Mungu yuko kazini. Kuna milango iliyo wazi katika miji, katika majimbo, katika nchi, na kubwa kuliko yote, katika mioyo ya watu binafsi . 


 Soma Matendo 8:26–38. Aya hizi zinatufundisha nini kuhusu usikivu wa Filipo kwa Mungu na utayari wake wa kutumia fursa zinazoletwa na Mungu? 


 " Malaika alimwongoza Filipo kwenda kwa mtu aliyekuwa akitafuta nuru na aliyekuwa tayari kupokea injili, na leo malaika wataongoza hatua za watendakazi watakaomruhusu Roho Mtakatifu atakase ndimi zao na anoe na kulainisha mioyo yao. Malaika aliyetumwa kwa Filipo angeweza kumhudumia Mwethiopia, lakini hii siyo njia ya Mungu ya kufanya kazi. Ni mpango Wake kuwa wanadamu wawahudumie wanadamu wenzao." –Ellen G. White, The Acts of the Apostles, uk. 109.


 Ikiwa tuna masikio ya kusikia na macho ya kuona, sisi, pia, tutaongozwa na malaika wasioonekana kuwafikia watafutaji wa ukweli wa ufalme.


 Angalia jinsi Maandiko yalivyokuwa kiini katika kisa hiki. Kadhalika, angalia jinsi ilivyokuwa muhimu katika kisa hiki kwa mtu aliyejua Maandiko kuyafafanua. Hapa tunajifunza nini ?

 BWANA AKUBARIKI SANA NA UWE NA TAFAKARI NJEMA

Post a Comment

0 Comments