KUHESABIWA HAKI KWA IMANI

Ndugu mpendwa nikukaribishe katika somo la Leo lisemalo:-

KUHESABIWA HAKI KWA IMANI

(Je Adamu na Hawa walihesabiwa haki Kwa imani?)

Kuhesabiwa haki kwa kifupi ni kunamaanisha kutohesabiwa dhambi au kusamehewa Biblia Inasema "Heri aliyesamehewa dhambi na kusitiriwa makosa yake. Heri Bwana asiyemhesabia dhambi.”(Zaburi 32:1, 2).
Tangu dhambi ilipoingia duniani, mwanadamu amekuwa akitafuta njia yake mwenyewe ya kujipatia haki na kujiokoa toka dhambini. Adamu na hawa walipoasi Bustanini walitafuta kujiokoa kwa kujifunika majani ya mti, jambo ambalo halikuwafaa, na hii ni Sawa na mtu anaye Hitaji kuhesabiwa haki kwa matendo au jitihada zake mwenyewe.

Lakini Kwa kuwa Mungu ni pendo akawapatia mavazi ya ngozi, ili kuonesha kuwa vazi halisi linaloweza kusitiri dhambi, linatolewana Yeye Mwenyewe pale Edeni. Na kwa njia hiyo Mungu alitangaza mpango Wake wa kumkomboa Adamu na uzao Wake kutoka dhambini. Alisema, “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na Uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” (Mwanzo 3:15.)

Swali!
Je Adam alihesabiwa haki Kwa Imani?


Wazazi wetu wa kwanza walipoanguka dhambini, Mungu alitangaza mpango Wake wa kuwaokoa na uzao wao, "Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake, huo utakupenda kichwa, na wewe utamponda kisigino" (Mwanzo 3:15).
Hii ilikua ni ahadi ya kwanza ya kumkomboa mwanadamu kutoka dhambini ahadi ya kwanza ya neema. Ni vema kuzingatia kwa makini jambo la msingi hapa. Mungu anaongea na Adamu baada ya kuanguka dhambini, na kile alichokuwa anastahili ni mauti ya milele kwa uasi wake. Lakini Mungu anaingilia kati kwa ahadi ya kumtoa mwanadamu kwa Shetani na kumrejesha Kwake tena.

Maandiko hayaoneshi kama Adamu na Hawa walifanya lolote ili Mungu awapatie wokovu na msamaha. Hakuna tendo lolote jema walilotenda, bali ulikua ni wema wa Mungu tu kwao. Kwa nini alilazimika kuweka uadui kati ya nyoka na mwanamke na uzao wao? Ni kwa sababu baada ya anguko nia ya Shetani Naya mwanadamu ilikuwa moja, nayo ni uasi na uadui juu ya Mungu, Biblia Inasema, “Kwa kuwa nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.”(Warumi 8:7)
Hivyo mwanadamu na Shetani wakawa marafiki lakini wote wawili wakawa maadui wa Mungu. Ndio sababu ili kumrejesha mwanadamu kwa Mungu, ilibidi urafiki kati yake (mwanadamu) na Shetani uvunjwe ili uadui na uasi wake juu ya sheria ya Mungu uondolewe, na apatanishwe na Mungu tena.

Kwa sababu wakati wa kutolewa kwa kafara halisi ya Kristo ulikua haujafika, Mungu alianzisha mpango kielelezo kwa njia ya kafara ya wanyama ili kuonesha kukubali na kupokea mpango huo.
Swali la kujiuliza, ni kwa nini ilikua ni lazima kafara ya wanyama? Kwa sababu uasi wa sheria ya Mungu ulidai uhai wa yule aliyeasi, na uhai uko katika hiyo damu. Lakini Mungu alimpatia mtu nafasi nyingine ya kuishi ambayo ndiyo rehema na mbadala wake, uhai mwingine ilibidi utolewe. Biblia inasema “Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; Nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi” (Walawi 17:11, pia aya ya 14 na Mwanzo 9:4). Ni kwa njia ya mauti au kuondolewa kwa uhai, kumwagika kwa damu ndipo sheria hutendewa haki na kuridhika.

Lakini pia ili ondoleo la dhambi lifanyike, ni lazima damu imwagike. Biblia inasema, "Pasipo damu hakuna ondoleo" (Waebrani 9:22). Walitakiwa kutoa kafara za wanyama kwa sababu ni kwa njia hiyo tu ndipo wangeonesha imani yao katika mpango wa Mungu wa wokovu kupitia kafara Yake Kuu ya Mwanakondoo achukuaye dhambi ya ulimwengu yaani "Yesu". Ndio maana kafara za wanyama zilikuwa kama kivuli zikimsonda kidole Kristo, maandiko yanasema, “Mambo hayo [yalikuwa] ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” "Maana haiwezi damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi." (Wakolosai 2:17; Waebrania 10:9).

Sasa basi Mungu anaona ni vyema mwanadamu akimbo lewes, Lakini Shetani alikusudia kuuvuruga mpango huu wa Mungu kwa kuanzisha mpango tofauti kupitia Kaini. Ukisoma Biblia yako (Mwanzo 4:4-7), utaona wote wawili wakiitikia agizo la kufanya ibada. Tofauti ni kuwa Habili anauamini na kuufata mpango wa Mungu wa wokovu, huku Kaini akiukataa mpango wa Mungu kwa kutoa kafara ya mazao ambayo ni matokeo ya kazi ya mikono yake mwenyewe, na hiki ni kielelezo cha wokovu kwa matendo!, aliitaji kuhesabiwa haki kwa Mungu, kupitia jitihada zake jambo halikubaliki na wala halina kibali mbele za Mungu.
Biblia inasema: "Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini, kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki. " Kwa imani alitoa dhabihu iliyo bora zaidi.
Hivyo ndivyo Shetani anavyofanya hata sasa kuwaongoza watu wafuate sehemu ya maagizo ya Mungu, na pia hubadilisha kwa namna wanavyoona ifaavyo kwao kama vile tu ilivyokuwa kwa Kaini (Angalia Mathayo 15:9 na Mithali 3:5-8).

Je waisraeli katika kukombolewa kwao hawakupata neema ya kuhesabiwa haki kwa imani?


Ni swali ambalo tunaweza kujiuliza, hivi Israel hawakuipata neema kama ilivyo sasa? Kama ndivyo je zile kafara za wanyama zilikuwa za nini? Kwanini mnyama aichukue mauti ya mdhambi?

Biblia Inasema "Iwapo ahadi ya Mungu ya kumkomboa mwanadamu ilikuwa ni kwa neema, na watu wote tangu Adamu hadi Ibrahimu walihubiriwa habari njema za wokovu katika Kristo Yesu" (Wagalatia 3:8); Je, Waisraeli walitakiwa kujiokoa wenyewe kwa matendo ya sheria? La hasha.

Biblia inasema "Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vilevile kama hao. "(Waebrania 4:2).

Naam habari njema ya wokovu tunayohubiriwa sisi leo, ndiyo ileile iliyohubiriwa kwa Adam, Nuhu, Ibrahimu na hata kwa Waisraeli. Kwa hiyo ni wazi kuwa kamwe Mungu hajawahi kufundisha mpango mwingine wa wokovu tofauti na ule alioupanga kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, yaani, wokovu kwa neema kwa njia ya imani katika Kristo Yesu (Waefeso 2:8).

Jambo hili lilifundishwa kwa kina katika mfumo wa kafara na huduma za patakatifu kwa Israel zamani. Kama ilivyo kuwa tangu Adamu, utoaji kafara za wanyama katika Israeli ulionesha imani yao kwa Mwanakondoo wa Mungu ambaye angelikuja baadaye, yaani Kristo.

Katika huduma zile za utoaji kafara, wakati mwenye dhambi alipokwenda na mnyama ili kutoa dhabihu, aliungama dhambi zake juu ya mnyama huyo.

Hilo lilikuwa tendo la imani lilofanya dhambi zihamishwe kutoka kwa mkosaji kwenda kwa mnyama, kisha mnyama yule alichinjwa, na kwa njia ya damu yake iliyonyunyizwa katika patakatifu, dhambi hizo zilihamishiwa kwenda patakatifu hadi siku ya upatanisho au hukumu.

Mnamo siku ya upatanisho kuhani mkuu alifanya upatanisho na utakaso kwa ajili ya dhambi zote zilizoungamwa kwa njia ya imani katika kipindi cha mwaka mzima, mdhambi aliamini kwamba dhambi zake zilikuwa zimefutwa kabisa kwa maana Bwana alikuwa amewaahidi wale wote ambao wangetimiza sharti hilo la imani (Walawi 16; 23:26-30).

Hivyo hakuna popote ambapo Mungu alimwambia mwanadamu kufanya upatanisho Naye au kujipatia haki kwa matendo ya sheria, kwa sababu ni Damu ya Yesu tu ndiyo inayoweza kutakasa dhambi , na Wala si matendo ya sheria. (Waebrania 9:14; 10:10).

Watu wa kipindi cha agano la kale walihesabiwa haki kutokana na imani yao kwa Masihi ajaye, ambaye aliwakilishwa na kafara za wanyama walizozitoa (Waebrania 9:1-10).

Agano la kale ni injili katika vielelezo au mifano, maneno ya Yesu mwenyewe yanathibitisha hilo:

“Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika Maandiko yote mambo yaliyomhusu Yeye Mwenyewe” (Luka 24:25-27).

Tena Yesu anaendelea kusema "Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa jinsi atakavyoiona siku Yangu, naye akaiona, akafurahi."(Yohana 8:56).

Naam, ni hakika kabisa kuwa watu wa agano la kale walihubiriwa na kuhesabiwa haki kwa imani, na wala si kwa matendo ya sheria. Madai ya kuokolewa kwa sheria ni upotoshaji wa ibilisi.

Je, kwa nini mwanadamu hawezi kamwe kuipata haki kwa njia ya utii wa sheria?

Barikiwa sana.....!!!

Post a Comment

0 Comments