🙏NINI MAANA YA SALA🙏


Sala ni kuinua moyo kwa Mungu au maombi ya mambo mema kwa Mungu.

Katika sala tunaukusanya moyo, tunajiingia ndani yetu kabisa kwa msukumo wa Roho Mtakatifu, tunaamusha imani ili kuingia ndani ya uwepo wa Mungu na kujikabidhi kabisa kwake yeye aliye chanzo cha uhai wetu.


Ndugu zangu wapendwa, ni ukweli usiopingika kuwa, kusali ni kuingia ndani ya moyo na kujitathimini kwa msaada wa mwanga wa Roho Mtakatifu na Neno la Mungu. Ni kupima jinsi gani tumeishi kwa uaminifu maagizo ya Mwenyezi Mungu. Kusali ni kujijua, kujitambua na kujenga uhusiano na Mungu kwa mwanga wa imani. Ni kujua madhaifu yetu na kuomba neema za Mungu ili aweze kutupa nguvu za kuyarekebisha. Mtu asiyesali ni mtu wa hatari sana, tena anapaswa kuogopwa kama "ukoma" au "virusi vya corona". Maisha ya mtu huyu muda mwingine huwa ni ya kushangaza kidogo, badala ya kuingia ndani ya moyo na kuyatafakari maisha yake, yeye hudhurura nje akitazama maisha ya watu wengine. Sifa za mtu huyo; huwa ni bingwa wa kulalamika na kuwakosoa watu wengine, na tena furaha yake ipo katika kuona makosa na madhaifu ya watu wengine yakifichuliwa wazi, lakini yeye ya kwake wala hana hata habari nayo.

Ndugu zangu wapendwa, kuna simulizi fulani linalosema kuwa; " "Umeme ukikatika katika nyumba ya mtu anayeishi Ulaya, kitu cha kwanza na cha haraka anachofanya mtu huyo ni kwenda ndani ya nyumba yake na kuona kama kuna kasoro au hitilafu imejitokeza, atajaribu kuangalia soketi vizuri kama haiko vizuri atajaribu kuirekebisha au kama bili imeisha atajaribu kuirekebisha nk. Lakini umeme ukikatika katika nyumba za Kiafrika, kitu cha kwanza afanyacho Mwafrika; ni kwenda nje ya nyumba yake na kuangalia nyumba za jirani zake kama nazo zimekatiwa umeme. Basi akiona hata na umeme umekatika kwa jirani mtu huyo walau hahuzuniki sana kwani, huamini ule msemo wa Wahenga kwamba; "Kifo cha wengi ni harusi" lakini kama kwa majirani umeme unawaka na kwake umekatika mtu huyo huona taabu kweli kweli."

Ndugu zangu wapendwa, ndivyo hata na sisi inavyotokea kwenye maisha yetu ya kiroho. Badala ya kurekebisha mapungufu yetu na kumwomba Mungu atuimarishe, tunazidi kukazia macho maisha ya watu wengine. Kumbe basi, maisha ya sala ni mwaliko wa kujitafakari na kubadilisha mwenendo wetu kwa kuyafananisha maisha yetu na maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo. Hata hivyo unabaki ukweli kwamba mwanadamu bado ana muda wa kusali na kujirudi kwa Muumba wake, nafasi yake ya kujirudi ndani na kujitathimini bado imeachwa wazi kwenye mikono yake mwenyewe. Mungu anamsubiri kama yule mwanampotevu ili amkumbatie kwa upendo na hivyo ndivyo anavyofanya Mwenyezi Mungu katika maisha yetu ya kila siku hasa maisha ya sala. Ndugu zangu, ni wazi kuwa, katika kusali, Mungu na mwanadamu wanakutana, Mwanadamu anamweleza Mungu haja zake na Mungu anasikiliza. Wakati huo huo naye Mungu anampa maagizo mwanadamu, naye huyo mwanadamu anatekeleza. Furaha ya Mungu bila shaka ni kuyaona maisha ya mwanadamu yakibadilika kwa kumrudia yeye, kwa kumpenda zaidi ya viumbe wengine wote sambamba na kuwapenda majirani kwa upendo wake.
KWA MAHITAJI YAKO YA

WEBSITES DESIGNING AND DEVELOPMENT, MOBILE APPS BUILDING, GRAPHICS DESIGNING, VIDEO EDITING AND CREATIVITY......CONTACT US +255 743 524 143/+255 657 014 782

MBIFILE CREATIONS...
KNOW MORE ABOUT US>>>

Mtu anaposali na akashindwa kubadili maisha yake hapa twasema kuwa, mtu huyo haelewi maana ya sala. Ndugu zangu wapendwa, inawezekana na sisi tukawa miongoni mwa watu ambao wanakuwa wakisali lakini tabia zetu mbaya zimekuwa zikiwachuza watu wengine. Basi kupitia makala hii tutaenda kuelewa kwa mapana na upembuzi wa kina kuhusu maana ya sala, tutaenda kujifunza uhusiano uliopo kati ya maisha yetu ya nje tunayoyaonesha kwa jamii inayotuzunguka na maisha yetu ya ndani ya sala, kwa hakika tutaelewa kuwa mtu anayesali vizuri huishi vizuri pia. Mbali na hayo tutajifunza; jinsi ya kupata fadhira za ki-Mungu, mitindo mbali mbali ya sala, maana ya unyenyekevu wa kweli, jinsi ya kutambua mapenzi ya Mungu, mambo muhimu ambayo mtu anayesali hukutana nayo, jinsi ya kukabiliana na madhaifu yetu, jinsi ya kushinda vishawishi, matunda ya sala ni yapi? nk. Ninawakaribisha wapendwa, tuweze kufungua mioyo yetu na kupokea kile ambacho nimewaandalia juu ya makala hii, katika sehemu hii inayohusu "Maana ya Sala". Nimewaandalia kisa cha bwana mmoja tajiri na kijana maskini mkata kuni, nitawaeleza kisa chenyewe na mwisho wa kisa hiki nitaomba tuweze kugundua maana ya sala.

"Kulikuwa na bwana mmoja tajiri aliyekuwa na nyumba nzuri lakini bwana huyo alikuwa mchaMungu. Bwana huyo alipenda sana kusali kila mara, ndipo basi hata na nyumbani mwake alimokuwa akiishi, aliamua kumjengea Mungu kikanisa kidogo ili aweze kuwa karibu naye zaidi. Baada ya kujenga kikanisa hapo nyumbani mwake alimwita Padri ili abariki, naye Padri hakufanya ajizi alibariki na kumtakia kila la kheri bwana huyo. Basi bwana huyo akawa kila siku akisali na kufurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake. Kwa muda maalum baada ya kuona Mungu yupo upande wake aliamua kumwuliza Mungu, "Hivi ee Mungu wangu katika eneo hili, ni nani zaidi anayekupendeza?" Bila shaka bwana yule alimwambia Bwana Mungu vile akitarajia kuwa Mungu angemjibu kuwa ni yeye. Basi, Mungu akamjibu, "KATIKA ENEO HILI UNALOISHI, NINAPENDEZWA NA YULE KIJANA MKATA KUNI ANAYEISHI KWENYE KIBANDA KARIBU NA NYUMBA YAKO NZURI" Yule bwana kusikia vile alishangaa sana akagutuka na kusema, "Huyo kijana mbona kila siku anaenda msituni asubuhi na kurudi jioni je, anakukumbuka mara ngapi?, mbona mimi nina sali muda wote na wewe unampendelea yule kijana badala yangu?" Mungu hakutaka kubishana naye bali alimwambia, "CHUKUA SAHANI ILIYOJAA MAFUTA YA KUPIKIA NA UZUNGUKE NAYO MPAKA KATIKA NYUMBA YA MWISHO YA PEMBEZONI MWA ENEO HILI NA UJITAHIDI HATA TONE MOJA LA MAFUTA LISIJE LIKADONDOKA NA UTAKAPORUDI NITAKUPA JIBU." Yule bwana akaenda na akajitahidi kufuata maelekezo aliyoambiwa na Mungu, njiani hakumwaga hata tone moja la mafuta hayo ya kupikia. Alifanikisha na akarudi kwa shangwe kwa Mungu na kumwambia, "Ee, Mungu wangu nimetimiza kile ulichoniambia" Mungu akamjibu, "ULIKUWA UNAFANYA NINI MUDA WOTE HUO?", yule bwana akamjibu, "Nilikuwa nashughulikia na kazi hii uliyonipa" Mungu akauliza tena, "NI MARA NGAPI ULISALI?" yule bwana kusikia hivyo alimwomba msamaha Mungu na kusema, "Samahami nilikuwa nimetingwa na kazi uliyonipa na nikasahau kusali" "VIZURI", Mungu alimjibu, " MTAZAME YULE MKATA KUNI, YUPO BUSY ANAFANYA KAZI YANGU LAKINI HUWA ANANIKUMBUKA WALAU MARA TATU KWA SIKU, NDIYO MAANA NIMEPENDEZWA NAYE."

Ndugu zangu wapendwa, tumejifunza nini katika kisa hiki? Je, tumepata walau tafsiri fulani juu ya sala?, Je, tumeelewa kuwa sala ni zaidi ya kushinda Kanisani, asubuhi mpaka jioni? Basi ninawasihi tuweze kuendelea kutafakari kisa hiki na baada ya kutafakari kwa kina ninaomba tuweze kutafuta maana ya sala kulingana na kile tulichojifunza kwenye kisa hiki.

Basi niwaachie tafakari hii iweze kutuongoza rej. (Zaburi. 15) "Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako? Ni nani atakayefanya maskani yake katika kilima chako kitakatifu? Ni mtu atendaye kwa ukamilifu, na kutenda haki; asemaye kweli kwa moyo wake. Asiyesingizia kwa ulimi wake, wala hakumtenda mwenziwe mabaya, wala hakumsengenya jirani yake. Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, bali huwaheshimu wamchao Bwana. Ingawa ameapa kwa hasara yake, hayabadili maneno yake. Hakutoa fedha yake apate kula riba, hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo, hataondoshwa milele."
-Neno la Bwana,...tumshukru Mungu.

Ndugu zangu wapendwa, tafakari hii itusaidie kwa karibu zaidi ili tuweze kuelewa maana ya sala kadri ya kisa chetu cha leo kuwa, Sala si tu hali ya mtu kushinda Kanisani asubuhi hadi jioni akiwa anaongea na Mungu. Bali pia hata katika shughuli zetu tuzifanyazo kila siku tunaweza kugundua uwepo wa Mungu, kwa maneno mengine ni kwamba, hata katika wingi wa shughuli zetu tunaweza kupata muda wa kusali.

Ndugu zangu, ninawatakia kheri na baraka tele katika maisha yenu, makala hii itusindikize katika maisha yakumfuasa Kristo aliyechanzo cha kwanza cha maisha ya kiroho, yeye yupo pamoja nasi daima. Amina.
Tumsifu Yesu Kristo...

Post a Comment

0 Comments