Wivu ni nia ovu dhidi ya mafanikio ya wengine. Ni kukosa nia njema kwa yule aliyefanikiwa kupata kile ambacho unatamani kuwa nacho na hivyo kumuona kama adui mshindani wako.
Wivu hutokana hasa na tabia ya ubinafsi wa mtu kutamani kuhodhi mafanikio na hata njia zake zote.
Wivu humfanya mtu kujenga chuki na uhasama kwa wale anaowatazama kama washindani wake kiutendaji. Mwenye wivu asingependa wengine wafanane naye au wapate kile alichonacho.
Mwenye wivu angetamani Mungu abebe tabia ya uchoyo na upendeleo yaani awanyime wengine ampe yeye tu.
Mungu wetu ni mwema na mkarimu kwetu sote wala hampendelei mtu bali humpa kila mmoja apendavyo yeye. Na ndiyo maana anataka usitamani vya mtu mwingine.
Tendea kazi alivyokupa Mungu, si kwa kutazama wengine wamepewa nini, na wanavitumiaje ili unung'unike kuwa Mungu amekosea kuwapa bora ungepewa wewe.
Wivu usipodhibitiwa huweza kutuingiza katika dhambi ya kumkufuru Mungu kwa kudhani anatudhulumu au kutunyang'anya vilivyo stahiki zetu na kuwapa wengine wasio stahiki.
Wivu usipotafutiwa tiba hutusukuma kuwachukia wengine, kupanga mipango mibaya dhidi yao, kuwaombea na kuwatakia mabaya, ushirikina na hata mauaji.
Wivu ni kiti cha majivuno, kiburi na ubinafsi ambavyo huleta uadui. Ni kinyume kabisa cha unyenyekevu kilicho kiti cha utii ambacho hutujengea urafiki madhubuti na watu.
Tunafanikiwa kwa neema ya Mungu tu na jitihada zetu ndogo ambazo si umiliki binafsi wa yale tuliyonayo bali tunapewa bila kustahili na hivyo wengine pia wanayo haki sawa kupata mbele ya Baba wa milele.
Usitafute kumuangusha mtu ili aonekane kuwa dhaifu kwako, bali muinue kudhihirisha nguvu yako.
0 Comments