Naomba kuondolewa utata kuhusu picha ya Yesu. Ninachanganywa na habari kwamba picha tulizo nazo si halisi bali kwamba ni za mwigizaji wa filamu ya Yesu Brian Deacon au ya Papa Mt. Alexander VI Cesare Borgia kwa vile ile ya mama Veronica ya uso wa Yesu ilishapotea mwaka 1527.
Jibu fupi: Acha nianze kwa kusahihisha jambo kabla ya kuendelea na jibu langu. Hakujapata kuwapo mtu anayeitwa Mt. Alexander VI Cesare Borgia. Ukweli ni kwamba alipata kuwako Cesare Borgia ambaye alikuwa mtoto wa Papa Alexander VI.
Sasa tuendelee. Kwa kujiondolea utata kuhusu picha ya Yesu inatupasa tujue kwamba wasanii wa kale walipata kujenga sura ya Yesu kwa kutumia masimulizi ya watu waliopata kukaa na Yesu na pia masimulizi ya kale kuhusiana na mwonekano wa vijana au wanaume wa Nazereti au Galilaya enzi za karne ya kwanza. Hivi tusichanganywe na habari za picha za akina Cesare Borgia na Brian Deacon. Wawili hao waliondokea sura zao kufanana na sura ya kuchongwa au kuchorwa ya Yesu Kristo.
Kama ni “foto” ya kamera basi yaweza kuwa ya mmoja wa watu hao, lakini kama ni ya kuchorwa au kuchongwa haitegemei sura za watu hao bali ni zao la fikra za wasanii wa awali zaidi. Wala tusizijali “foto”. Kwa vyovyote, kazi za kuchongwa au kuchorwa zinahitaji heshima kwa vile zinatusaidia kumtafakari Yesu asiyeonekana maana vichwa vyetu siku zote husaidiwa na milango ya maarifa, macho, pua na kadhalika. Kuazibudu picha kama kunafanyika ni kwa bahati mbaya sana nako lazima kunatokana na ukufi wa uelewa. Kwa vyovyote si mafundisho ya Kanisa Katoliki.
Picha aliyoachiwa mama Veronica ilishapotea mapema zaidi na wala siyo katika mwaka 1527. Ingekuwapo hadi mwaka 1527 wanadamu tusingelikosa nakala yake kwani shughuli za uchoraji na uchongaji zilishastawi sana huko Ulaya.
Jibu refu: Ni kweli kuna mkanganyiko kuhusiana na picha ya Yesu. Kumbe yafaa leo tuambizane inavyotakiwa mambo yaeleweke. Ni hivi, enzi za karne ya kwanza Baada ya Kristo, Kristo alipokuwa akiishi mubashara, hakukuwa na teknolojia ya kamera. Badala yake, watu walitegemea uchoraji picha na uchongaji sanamu. Kwa bahati mbaya, kwa sababu ya kutokujua kwamba watu watakuja kuhitaji picha au sanamu halisi ya Yesu Kristo, hakuna mchoraji wala mchongaji aliyemchora ama kumchonga Yesu.
Lakini, miaka mingi baada ya kufa na kufufuka kwake watu walitamani kupata picha au sanamu ya Yesu. Juhudi za kupata sura halisi na sanamu halisi hazikuzaa matunda maana ile leso aliyoachiwa Veronika ilikuwa haijulikani iliko na wala habari za sanda ya Yesu hazikuwa na ukweli wa mashiko. Kitambaa kinachojulikana kama “Sanda ya Yesu” au “Sanda ya Torino” kipo huko Torino, Italia, lakini ni ugunduzi wa mwaka 1390 na hadi sasa hakuna makubaliano mahsusi juu ya ukweli wake.
Askofu wa Torino alishasema ni sanda iliyogushiwa ingawa mintarafu sura Papa Pio XII, mwaka 1958, aliikubali kama inayosadifiana na ya Yesu. Katika hali hii, uwapo wa sanda hii si kati ya mafundisho msingi ya Kanisa. Anayetaka anaweza kuisadiki, asiyetaka anaweza kuachana nayo, ruksa tu!
Jinsi Sura ya Yesu Ilivyofikiwa kwa Sanaa
Sura ya Yesu ilipambazuka vichwani mwa wachoraji na wachongaji kufuatia mambo mawili: masimulizi ya watu waliopata kuishi naye na masimulizi juu ya mwonekano wa vijana katika karne ya kwanza huko Nazareti na Galilaya.
Sura ya Yesu kwa Masimulizi ya Watu wa Kale
Kwa kuwa Yesu hakuishi peke yake duniani, watu walimwona, kukaa naye, kula naye na hata kumgusa, picha ya Yesu ilikuwa inasimuliwa. Ndipo wachoraji au wachongaji walipoanzia. Walianzia kwenye masimulizi hayo. Ni kama mtu akusimulie habari za baba wa baba yako, yaani babu yako, ambaye hukumwona. Masimulizi ya mtu aliyepata kumwona baba wa baba yako ambaye hukupata kumwona yanaweza kukupa picha yake fulani. Aidha, mtu yule akisema kwamba sura na mambo ya babu yako yaliendana na vijana wa wakati wake, picha yake itapambazuka zaidi kichwani mwako ukijua vijana wa wakati wake walikuwaje au walikuwa wanapendelea nini. Ndivyo sura ya Yesu ilivyoanza kupambazuka vichwani mwa wachongaji na wachoraji.
Mwonekano wa Vijana Katika Karne ya Kwanza
Watu husimulia mwonekano wa vijana wa karne ya kwanza wa huko Nazareti au Galilaya. Kumbe, ndivyo picha au sura ya Yesu ilivyoanza kupambazuka vichwani mwa wasanii, yaani kwa kutilia maanani mwonekano wa vijana na wanaume wa karne ile ya kwanza. Mwonekano huo unaelezeka ifuatavyo:
i. Kichwa, Nywele na Ndevu
Katika karne ya kwanza inasimuliwa vijana wa Kiyahudi, huko Nazareti au Galilaya, walikuwa wanaacha nywele ndefu na ndevu za wastani, si ndefu sana wala fupi sana. Nywele na ndevu, vyote walikuwa wanapendelea kuvichana kati na kuzimwaga katika pande mbili. Wanamaanisha walikuwa wanaweka mgawanyo (way) ili nywele kichwani ziangukie pande mbili na hali kadhalika ndevu ziwe pande mbili. Kumbe, huu ndio mwonekano walioudaka wasanii na wachoraji kutika kuichora sura au kuichonga sanamu ya Yesu. Kumbe, kwa kufuatia sura au picha hii yeyote anayetunza nywele na kuzifanyia hivyo, kwa namna fulani, atafanana na Yesu, siyo Yesu kufanana na mtu huyo. Tuelewe jambo hili vyema sana.
*ii. Mavazi ya Wayahudi katika Karne ya Kwanza*
Walivyokuwa wakivaa watu enzi zile za karne ya kwanza ndivyo walivyokuwa wanavaa Yesu na mitume na wafuasi wake. Yesu, mitume na wafuasi wake hawakuja na mitindo mipya ya mavazi. Hivi swali, walikuwa wanavaaje, yatosha kufafanua walivyokuwa vijana au wanaume Wayahudi enzi za karne ya kwanza Baada ya Kristo.
Vijana na wanaume wakati ule walikuwa wanavaa vitu rahisi vya aina tano au sita (rej. Yn 19:23).
(i) Shati (yaani kanzu fupi, hii ndiyo iliyotumika pia kama chupi) chini ya kanzu ndefu ambayo ilikuwa ya kawaida enzi hizo (rej. Yn 13:4 Yesu aliweka kando nguo zake kabla ya kuwaosha mitume miguu yao).
(ii) Kanzu ya Yesu Kristo haikuwa na mshono (rej. Yn 19:23).
(iii) Mshipi laini wa kufungia kanzu kiunoni. Kulikuwa na uwezekano wa kuuzungusha mshipi kiunoni mara kadhaa.
(iv) Vazi la juu, yaani joho (kwa kawaida nguo ya sufu nyeupe, nguo ya aina na umbo la kawaida rej. Mk 9:3). Nguo za wakati ule zilikuwa nyeupe, lakini si weupe wa kustaajabisha. Joho la Yesu bila shaka lilikuwa na matamvua ya kawaida kama inavyosomeka katika Hes 15:37 – 41.
(v) Makubasi miguuni (rej. Mt 3:11). Viatu vya kutumbukiza miguu vilikuwa nadra kabisa.
(vi) Kilemba (kilikuwa kama mtandio laini wa kawaida uliozungushiwa kichwani). Bila shaka Yesu alikuwa na kilemba chake kwa sababu kwa wakati ule hakuna mwalimu wa Kiyahudi aliyekuwa akitokea mbele ya watu na kichwa kisichopigwa kilemba.
Maoni na Mtazamo wa Kiyahudi kwa Mjumbe wa Mungu
Wayahudi walikuwa na maoni maalumu juu ya mwonekano wa mtu aliyetumwa na Mungu. Kifupi, walikuwa wanampokea mtu kama mjumbe wa Mungu kwa vigezo vitatu: mwonekano wake, uwapo wa mashahidi na uwapo wa ushahidi.
Mintarafu mwonekano, Wayuhudi walikuwa wanampokea mwanaume mrefu na mzuri wa sura kama mjumbe wa Mungu. Kazi za kuchaguliwa kama ukuhani mkuu zilitilia maanani jambo hili. Hivi ukisikia kwamba kulikuwa na Anasi au Kayafa makuhani wakuu, pata picha ya watu warefu, wazuri na wasio na vilema vyovyote, maana vinginevyo wasingechaguliwa. Kinyume cha sifa za urefu, uzuri na kutokuwa na kilema, mwanaume mfupi, mwenye sura mbaya au kilema alikuwa akikataliwa au alipata taabu sana kupokelewa kama mjumbe wa Mungu.
Hapa elewa maana ya mwiba wa Mtume Paulo (2Kor 12:7). Yaonekana Paulo alikuwa mfupi na mwenye ugonjwa wa macho, wataalamu wanadhani “trachoma” (Gal 4:15), ndiyo maana watu walikuwa wanasema wanapomwona Paulo ana kwa ana hakuwa lolote (2Kor 10:10) na yeye mwenyewe alikuwa akikazana kumwomba Mungu aondolewe mwiba huo kwa muujiza labda wa kurefushwa na kuponywa ugonjwa wake.
Tunajua Mtume Paulo alizoea kuomba kuondolewa mwiba huo mpaka alipoambiwa na Mungu aachane na maombi ya namna hiyo kwa maana neema yake ilikuwa inamtosha (2Kor 12:9).
(Kuhusu mashahidi, mjumbe wa Mungu alitakiwa awe anashuhudiwa walau na mwanaume mmoja, si wanawake, watoto au wendawazimu, hata kama wangekuwa maelfu. Yesu alikuwa na shahidi wake. Yesu mwanaume alikuwa anashuhudiwa na Mungu, Baba yake, ambaye alikuwa mwanaume mwenziwe, tazama Yn 8:16-18. Na hiki ndicho kisa Yesu aliwatuma mitume au wafuasi wawili wawili. Yaani mmoja akiwa anahutubu, mwingine awe shahidi wake.
Kuhusu ushahidi mjumbe wa Mungu alitakiwa kuwa na uwezo wa kutenda miujiza. Ndiyo maana hata Yesu alikuwa anadaiwa aoneshe ishara ili wamwamini. Yesu alifanya miujiza mingi na ilitosheleza kama ushahidi (rej. Yn 6:30).
Hivi, kutokana na maoni na msimamo wa Wayahudi, mintarafu wajumbe wa Mungu, Yesu lazima alikuwa mrefu, mzuri na asiye na kilema chochote, la sivyo, watu wangemnyanyapaa kama walivyokuwa wanamnyanyapaa Mtume Paulo. Aidha, siyo tu Yesu hakuwa na kilema cha kuchafua sura yake bali alikuwa na nguvu na siha tele ndiyo kisa aliweza kumudu kwenda huko na huko kwa miguu. Kwa sababu hii, mchoraji au mchongaji yeyote wa sura ya Yesu lazima alipambazukiwa kichwani mwake kumchora au kumchonga Yesu mrefu na mwenye sura ya kupendeza, mwenye nguvu na siha njema.
Picha na Sanamu Zilikuwa Kabla ya Akina Cesare Borgia na Brian Deacon
Picha na sanamu za Yesu na zinginezo zilikuwapo hata kabla ya akina Cesare Borgia na Brian Deacon kuzaliwa. Ndiyo kisa mgogoro wa picha na sanamu, uliojulikana kama “iconoclasm” ulitokea kwenye Kanisa la Bynzatine kwa awamu mbili. Kutokana na watu kuzikataa picha na sanamu, picha na sanamu nyingi ziliharibiwa na kuchomwa moto. Awamu ya kwanza ilikuwa kati ya mwaka 726 na 787 na awamu ta pili kati ya mwaka 814 na 842 Baada ya Kristo. Lakini Kanisa lilikaa chini kwenye Mtaguso wa Nicea II (mwaka 787) na kutuliza mzuka wa mashabiki wa mgogoro huo kwa kuwajulisha kwamba picha na sanamu zilikuwa kwa ajili ya kusaidia akili za binadamu kutafakari mambo ya kiroho na owa[o wa wahusika wa kale na siyo kwa kwa ajili ya kuziabudu. Heshima kwa sanamu na picha huitwa kwa Kilatini “dulia” wakati ibada ni kwa Mungu tu (kwa Kilatini huitwa “latria”).
Sura ya Cesare Borgia
Sasa tugeukie sura za watu waliopata kufanana sura na sura ya Yesu wa kuchongwa au kuchorwa. Tuanze na Cesare Borgia na mwishowe tumalizie maelezo na Brian Deacon.
Hii ndiyo picha ya Cesare Borgia
Cesare Borgia alikuwa mwanasiasa, Mwitaliano mtawala wa Valentinois, mtu wa familia bora na kardinali mwenye asili ya Aragone na Italia, ambaye kugombania kwake madaraka kulimchochea Michiavelli kuandika kazi iliyoitwa MWANA WA MFALME. Cesare Borgia alikuwa mtoto wa Papa Alexander VI na kimada chake cha muda mrefu Vannozza dei Cattanei.
Cesare Borgia alizaliwa 13, Septemba, 1475, Roma, Italia. Alikufa 12 Machi, 1507 huko Viana, Uhispania. Mwenza wake wa ndoa alikuwa Charlotte of Albret (mwaka 1499). Tarehe 11 Machi, 2007, alizikwa upya katika kanisa la la Mt. María de Viana, huko Moreta, Uhispania.
Sura ya mtu mtu huyu ilipata kufanana kwa namna fulani na sura ya Yesu wa kuchorwa au wa kuchongwa kwa kadiri wasanii walivyokuwa wamemchonga au kumchora Yesu kutegemea masimulizi ya watu waliopata kumwona na kukaa na Yesu na vile vile kutegemeana na masimulizi ya mwonekano wa vijana na wanaume wa Nazareti au Galilaya katika enzi zake. Kwa namna hii si Yesu aliyefanana na Cesare Borgia.
Sura ya Brian Deacon
Sasa tuigeukie sura ya mwigizaji Brian Deacon. Kwa nia ya kutengeneza filamu ya mateso ya Yesu, wahusika walitafuta sura ya mtu aliyefanana na picha ya Yesu ya kuchorwa au kuchongwa. Ndipo wanaume walifuga ndevu na kuchujwa. Kati ya watu waliojitokeza, alishinda Brian Deacon.
Jinsi Brian Deacon alivyoonekana katika filamu, baada ya kuotesha ndevu kujifananisha na picha za kale za Yesu.
Hii ndiyo sura ya Brian Deacon akielekea kuzeeka. Siku hizi amezeeka zaidi.
Brian Deacon alikuwa mwigizaji Muingereza. Umaarufu wa mwigizaji huyu ulianza hasa mwaka 1979 alipokuwa mhusika wa mkuu wa filamu iliyojulikana kama JESUS iliyotengenezwa na shirika la uinjilishaji lililojulikana kama Mradi wa Filamu ya Yesu. Brian Deacon alichaguliwa awe mhusika mkuu kati ya waigizaji 263 waliojaribiwa na mtengenezaji filamu John Heyman.
Kifupi, Brian Deacon alizaliwa 13 Februari, 1949 mjini Oxford, Uingereza. (Sasa ana umri miaka 70). Urefu wake ni mita 1.73. mwaka 1998 alimwoa Nathalie Bloch-Lainé, wakati kati ya mwaka 1977 na 1987 alikuwa amemwoa Rula Lenska. Yeye ni baba wa Lara Parker Deacon. Kwa Brian filamu ya JESUS si ya kwanza kushiriki kuicheza. Ameshiriki pia vipindi vya televisheni The Feathered Serpent, Lillie, Good Girl, The Emigrants na Bleak House.
Je, Cesare Borgia na Brian Deacon Wamefanana na Yesu?
Hapana hawajafanana naye ila wao wamefanana na sura ya Yesu iliyofikiwa kwa mawazo ya wachoraji na wachongaji wa kale kabla Cesare Borgia na Brian Deacon hawajazaliwa. Kwa maneno mengine, sura za watu wawili hawa zilifanana na picha za Yesu zilizochorwa au kuchongwa zamani kabla ya kuzaliwa kwao. Hivi si sawa watu wanaposema eti sura ya Yesu ni ya Cesare Borgia na Brian Deacon wakati ni wao Cesare Borgia na Brian Deacon waliofanana na Yesu wa kuchorwa au wa kuchongwa.
Sikiliza. Mtoto hawezi kuzaliwa mwaka huu tukasema mama yake amefanana na yeye, badala ya kusema mtoto amefanana na mama yake, kwa vile mama yake alizaliwa kabla ya mtoto wake. Vivyo hivyo, mtu hawezi kuzaliwa leo tukasema Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amefanana na mtu huyo, badala yake haki itakuwa tuseme mtu huyo amefanana na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa sababu Nyerere aliishi kabla yake. Aidha, mtu hawezi kuzaliwa leo tukasema Mkwawa amefanana na mtu huyo, badala ya kusema mtu huyo amefanana na Mkwawa kwa sababu Mkwawa aliishi kabla ya mtu huyo.
Je, Wakristo Wanaabudu Picha za Cesare Borgia na Brian Deacon?
Hakuna anayeziabudu picha au sura za wawili hao. Labda kwa wale wasiojua picha za Yesu zina maana gani na zilianzaje. Kama kuna mtu anayeziabudu picha hizo, ni shauri lake wala si mafundisho ya Kanisa Katoliki.
Picha katika Sanda ya Torino
Sasa tumalizie na suala la ziada. Kuna kitu kinaitwa SANDA YA TORINO au SANDA YA YESU. Sanda hiyo inaonesha sura ya mtu ambaye alivishwa sanda hiyo. Sura ya marehemu huyo inafanana na sura ya Yesu wa kuchongwa au kuchorwa kama ilivyojengwa na wasanii wa kale. Itazame hapa chini.
Hii ndiyo Sanda ya Torino.
Ukweli wa Sanda ya Torino Unagomba
Sanda ya Torino imepimwa mara nyingi kwa kipimo cha vitu vya kale kinachoitwa “carbon dating”. Kwa mujibu wa vipimo hivyo, Sanda ya Torino ni ya mwaka 1390 na kuna mashaka kwamba ni ya kutengenezwa na matapeli. Kipimo cha vitu vya kale kinaonesha ni ya mwaka 1390 tu. Kanisa halijatamka kwamba ni ya kweli. Kwa hiyo si lazima kuisadiki kama kitu kinachotuletea sura halisi ya Yesu Kristo. askofu wa Torino alishasema ni sanda ya kughushiwa na tapeli mmoja alishakiriri kuigushi.
Hatima
Sasa tuhitimishe swali hili kamambe. Kwa kujiondolea utata kuhusu picha ya Yesu inatupasa tujue kwamba wasanii wa kale walipata kujenga sura ya Yesu kwa kutumia masimulizi ya watu waliopata kukaa na Yesu na pia masimulizi ya kale kuhusiana na mwonekano wa vijana au wanaume wa Nazereti au Galilaya enzi za karne ya kwanza. Hivi tusichanganywe na habari za picha za akina Cesare Borgia na Brian Deacon. Wawili hao waliondokea sura zao kufanana na sura ya kuchongwa au kuchorwa ya Yesu Kristo.
Kama ni “foto” ya kamera basi yaweza kuwa ya mmoja wa watu hao, lakini kama ni ya kuchorwa au kuchongwa haitegemei sura za watu hao bali ni zao la fikra za wasanii wa awali zaidi. Wala tusizijali “foto”. Kwa vyovyote, kazi za kuchongwa au kuchorwa zinahitaji heshima kwa vile zinatusaidia kumtafakari Yesu asiyeonekana maana vichwa vyetu siku zote husaidiwa na milango ya maarifa, macho, pua na kadhalika. Kuazibudu picha kama kunafanyika ni kwa bahati mbaya sana nako lazima kunatokana na ukufi wa uelewa. Kwa vyovyote si mafundisho ya Kanisa Katoliki.
Picha aliyoachiwa mama Veronica ilishapotea mapema zaidi na wala siyo katika mwaka 1527. Ingekuwapo hadi mwaka 1527 wanadamu tusingelikosa nakala yake kwani shughuli za uchoraji na uchongaji zilishastawi sana huko Ulaya.
0 Comments