WANANDOA WALIONG'ANG'ANIA TALAKA



Jaji mmoja anasimulia kuhusu tukio moja la wanandoa waliotaka kuachana. Mke ndiye aliyetaka talaka.

Katika kikao cha kwanza, jaji alisogeza mbele siku ya kutoa hukumu ili kuwapa fursa wahusika ya kupatana. Katika kikao kilichofuata akawauliza: "Bado mna nia ya kuachana?" Wakajibu: "Ndiyo, tunataka kuachana hata leo."

Kwa mara nyingine, jaji alisogeza mbele kesi yao huku wahusika wakionekana kuudhika sana kwa sababu walitaka kuvunja ndoa yao kila mtu awe huru. Jaji aliahirisha kesi hiyo mara nyingi.

Mwisho aliitisha kesi hiyo ambapo siku hiyo alimtaka mwanaume akae kwenye kiti na meza kisha aandike mazuri 10 ya mkewe. Mazuri 10 tu.

Aliwaambia kuwa yeye binafsi hatasoma walichoandika, bali wao wenyewe ndio watakaosoma, na akawataka waandike bila soni.

Baada ya mume kumaliza kuandika, jaji akamtaka mke asome taratibu na kwa siri, bila kutoa sauti. 

Mke alianza kusoma, akamtazama mumewe usoni na kuanza kutabasamu. Tabasamu likaongezeka.

Mara anamtazama mumewe kwa jicho la soni, mara anaitazama miguu ya mume, mara anamkazia macho. Muda wote huo mume naye anamtazama huku tabasamu likishamili usoni mwake.

Kisha ikaja zamu ya mke kuandika mazuri ya mume. Alipomaliza kuandika, mume alianza kusoma huku akitabasamu na kumtazama kwa umakini mkewe. Mara amtazame usoni, mara atazame chini.

Hakimu huyo anasema: "Nilikuwa nimekaa mimi na wao tu. Ikabidi nitoke ukumbini kwa dakika kadhaa. Niliporejea nilisikia minong'ono ya kulaumiana kwa upendo.

Niliwaambia kuwa wanaweza kutoka, warudi siku ya pili ambapo nitatoa hukumu kama wanavyopenda. Wakakubali.

Waliporudi siku ya pili walikuwa wameshikana mikono huku wakitabasamu."

Aliwauliza: "Je, niruhusu talaka?"

Wakasema: "Hapana. Jana tulipatana, tulimaliza matatizo yote na tumerejesha upendo wetu."

Hakimu anasema: "Mpaka sasa sijui walichoandikiana na wala nyinyi hamjui pia."

Kaka yangu, yatazame mazuri ya mkeo. Nawe dada yangu yatazame mazuri ya mumeo.

Yatazameni mazuri ya marafiki, ndugu na wale wanaowazunguka, maisha yenu yatageuka kuwa maridhawa.

Tunaweza kuzibadilisha changamoto za ndoa zetu na kupata suluhisho la kudumu kwa kupitia mazuri ya wenzetu. Hii ni njia ambayo imepata mafanikio makubwa sana katika mafunzo yangu ya Ndoa Maridhawa.

Post a Comment

0 Comments